Mbunge
wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amemtuhumu Mbunge wa
Monduli Edward Lowassa kwamba anahusika na kipigo alichokipata kutokana
na chuki aliyonayo kwake. Aidha
amemtuhumu Spika wa Bunge, Anne Makinda kwamba naye ni miongoni mwa
watu wanaomchukia pamoja na viongozi wengine wa Bunge, kwa kuwa hakuna
kati yao aliyempigia simu au kumtumia ujumbe wa kumjulia hali kutokana
na kipigo alichopata ambacho kimemsababishia maumivu makali. Akizungumza
jana akiwa kwenye chumba alicholazwa katika Taasisi ya Tiba ya Magonjwa
ya Mifupa na Ufahamu Muhimbili (Moi), Nassari alidai Lowassa ambaye
amewahi kuwa waziri mkuu kabla ya kujiuzulu, amemchukia tangu
alipomshinda mkwewe Sioi Sumari, kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge
uliofanyika Aprili mwaka jana.
Nassari
aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Selian ya jijini Arusha kabla ya
kuhamishiwa MOI, alidai kupigwa na kuchaniwa nguo na Green Guard wakati
alipokuwa katika jitihada zake za kuhesabu kura kwenye uchaguzi wa
udiwani wa Kata ya Makuyuni-Monduli. “Kipigo
nilichopata Lowassa anahusika ananichukia, anataka urais lakini hawezi
kuupata kwa kuuumiza watu kama hivi, alifikiri kwamba nitakufa sitakufa
hadi kwa mapenzi ya Mungu,” alisema. Alisema
kuna jambo ambalo wananchi wanapaswa kulifikiria ni jinsi ambavyo
kumekuwa na matukio ya kutekwa na kuvamiwa, lakini hakuna yanayohusisha
kiongozi wa CCM, badala yake ni raia wa kawaida na viongozi wa dini na
siasa. Nassari alidai akiwa kama wakala mkuu wa Chadema katika kata
hiyo, alikumbana na mambo kadhaa yaliyomshangaza, ikiwa ni pamoja na
kufanyiwa jaribio la kutekwa mara mbili, kabla ya kushambuliwa kwa
kipigo.
Hata
hivyo, Lowassa alipotafutwa kuhusiana na tuhuma hizo alikataa
kuzungumzia suala hilo na kusema hilo aulizwe Msimamizi wa Uchaguzi,
Paulo Kitaleki. Mwananchi
ilimtafuta Kitaleki ambaye pia ni katibu tarafa, alikanusha kuhusika
kwa Lowassa akielezea kuwa siku ya tukio hilo alikuwa Geita. “Huyu
Nassari ni mwigizaji na anafaa kuwa msanii kwa kuwa anaigiza tu hata
hakupigwa, bali yeye ndiyo aliyempiga Wakala wa CCM, Hussein Osama
ambaye ni mlemavu, kisha akatimua mbio baada ya vijana kutaka kumkamata,
nashangaa kumwona yupo hospitali akidai kupigwa, siyo kweli,” alisema
Kitaleki.
No comments:
Post a Comment