Jeshi la Polisi nchini limemtia
mbaroni mtu mmoja mjini Mbeya anayedaiwa kuhusika na vitendo vya ugaidi
akiwa na hati mbili za kusafiria, na mwingine Mtanzania adakwa akidaiwa
kusaidiana naye.
Mtu huyo aliyekamatwa wilayani Kyela, pia anatuhumiwa kuhusika na vitendo vya ugaidi nchini Uingereza.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI),
Robert Manumba, alisema mtuhumiwa huyo alikuwa anatumia majina mawili
tofauti kwenye hati za kusafiria na alikuwa akijaribu kuvuka mpaka wa
Tanzania kuelekea Malawi.
Alisema mtuhumiwa huyo alitumia hati
ya Tanzania yenye namba AB 651926 yenye jina la Adil Ally Patel na hati
ya Uingereza yenye namba NO 51555382 yenye jina la Iqbal Hassan Ally.
Manumba alisema hati ya Tanzania aliyokamatwa nayo ni kati ya hati 26 zilizoibiwa kwenye Ofisi za Uhamiaji mwaka mmoja uliopita.
Alisema mshukiwa wa ugaidi alikuwa
akisaidiwa na Mtanzania mmoja ambaye hakumtaja jina na baada ya
kukaguliwa kompyuta mpakato (laptop) yake ilikuwa na maneno ya uchochezi
ya kidini kuhusu imani tofauti.
Manumba alisema aliwasiliana na
Serikali ya Uingereza kuhusu hati ya mtuhumiwa huyo na kuelezwa kuwa ni
halali na kufahamishwa kuwa mtu huyo wanamtafuta kwa tukio la ugaidi
nchini Uingereza.
Alisema kuna Mtanzania mwingine
ambaye hakumtaja jina, alikamatwa kwa kuhisiwa kujihusisha na mtuhumiwa
huyo wa ugaidi ambaye baada ya kukaguliwa pia alikutwa na kompyuta yenye
maneno ya uchochezi dhidi ya dini isiyomhusu.
Alisema mtuhumiwa huyo alijitambulisa kuwa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo kimoja kilichopo nchini Sudan.
Manumba aliwataka wazazi kuwa
waangalifu na vijana wao wanaokwenda kusoma nje ya nchi kwa kuwa baadhi
yao hurubuniwa na kujiingiza katika mambo yanayohusiana na ugaidi.
Aliongeza kuwa polisi wana uhakika
kwamba kuna baadhi ya vikundi vya kigaidi ndani ya nchi ambavyo vina
mipango ya siri ya kutekeleza ugadi nchini.
Aliwataka Watanzania kuwa waangalifu
wakati polisi ikifanya kazi yake ya uchunguzi na kuonyesha kuwa hali ya
usalama si nzuri nchini kutokana na matukio ya kihalifu yanayoendelea.
Aidha, alisema polisi inaendelea na
uchunguzi dhidi ya matukio ya mlipuko miwili ya mabomu iliyotokea mkoani
Arusha na lile la kuuawa kwa Padri Evarist Mushi, Zanzibar.
Alisema matukio hayo yameonyesha sura mbaya kwa Tanzania ya kuwepo kwa tishio la ugaidi.
Alisema uchunguzi utakapokamilika washitakiwa watafikishwa kwemnye mikono ya sheria kuhukumiwa kwa makosa ya jinai.
Aliongeza kuwa taarifa zitakazokuwa
zikitolewa na raia wema zitasaidia polisi kurahisisha uchunguzi na
kuwakamata wahusika kwa wakati.
Manumba ametahadharisha kuwa ongezeko
la uhalifu nchini limekuwa likihusisha baadhi ya wananchi kutumika
vibaya na wavunjifu wa amani.
Alisema kufuatia matukio hayo, baadhi
ya watuhumiwa wanashikiliwa na baada ya uchunguzi kukamilika hatua kali
zitachukuliwa dhidi yao.
“Hii ni sifa mbaya Watanzania
wanapaswa kujiepusha na vishawishi vya aina yoyote vitakavyopelekea
kuvunjika kwa amani iliyopo tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanzania,”
alisema.
Katika matukio ya kigaidi yaliyotokea
siku za hivi karibuni watu watatu walikufa na zaidi ya 70 kujeruhiwa
baada ya kurushwa bomu kanisani na mtu asiyefahamika katika kanisa la
Katoliki Jimbo Kuu la Arusha wakiwa wamejumuika katika uzinduzi wa
Kanisa la Mtakatifu Joseph, Parokia ya Olasiti.
Katika tukio jingine jijini humo,
bomu lilipuka kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) eneo la Soweto kata ya Kaloleni mkoani Arusha.
Katika tukio hilo watu watatu
walifariki dunia kutokana na mlipuko wa bomu wakati chama hicho kikiwa
kwenye mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani.
Wakati huo huo Manumba alisema polisi
jijini Dar es Salaam limekamata meno ya tembo 347 katika eneo la Kimara
ambayo yanaamika yamepatikana kwa njia za kijangili katika mbuga za
Tanzania.
Alisema mbali na nyara hizo, kuna
meno mengine ya tembo 788 yalikamatwa nchini Malawi katika mji wa Mzuzu
na kwamba inaamika kuwa yalisafirishwa kutoka Tanzania kama mzigo wa
saruji kutoka katika kiwanda cha Saruji Mbeya.
Manumba alisema polisi nchini
wanafanyakazi kwa kushirikiana na polisi wa kimataifa kuhakikisha kuwa
ukweli wa matukio yanakuwa wazi na uchunguzi ukikamilika wahusika
watafikishwa katika vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment